Papa Leo XIV, amegunduliwa kuwa na saratani ya mapafu, licha kufanyiwa upasuaji na kuondolewa uvimbe mdogo kwenye pafu lake la kulia. Hayo yametangazwa na Vatican.
Leo mwenye umri wa miaka 71, alifanyiwa upasuaji siku ya Jumanne uliodumu dakika 90, katika hospitali ya kifahari ya Gemelli Jijini Rome, ambayo imewatibu viongozi hao wa kanisa katoliki kwa miongo kadhaa.
“Upasuaji huo ulifaulu na hakukuwa na hitilafu zozote. Baada ya upasuaji huo, Papa aliamka kawaida na kurejea kuchumbani mwake,” ilisema Vatican.
Uvimbe huo uligunduliwa wakati wa uchunguzi wa kawaida wa kiafya kwa mujibu wa Vatican. Papa Leo anatarajiwa kukaa hospitalini kwa muda wa wiki mbili.
Mnamo siku ya Jumapili kwenye mahubiri yake, Leo XIV alitangaza atafanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe kwenye moja ya mapafu yake.