Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imemkamata mwalimu kwa madai ya kuitisha hongo kutoka kwa walimu ambao hawana ajira, akisingizia atafanikisha uajiri wao kwenye Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC).
Lilian Nelima Buluma, ambaye ni mwalimu katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Friends School Kamusinga, kaunti ya Bungoma, alikamatwa baada ya uchunguzi wa awali kubainisha aliitisha hongo ya jumla ya shilingi 300,000 kutoka kwa walimu watatu watatu wanaotafuta ajira.
Mshukiwa huyo anadaiwa alipokea shilingi 150,000 kupitia M-Pesa kama sehemu ya fedha alizoitisha, akidai anauhusiano na tume ya TSC na maafisa wengine serikalini, kuwezesha watatu hao wapate ajira.
Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Bungoma, akisubiri kufikishwa mahakamani.
“Mshukiwa huyo anatafunguliwa mashtaka ya kuitisha na kupokea hongo,” ilisema EACC kwenye ukurasa wa X.