Vanessa Handas kuwakilisha Kenya kwenye Miss Africa Golden

Shindano hilo maarufu la bara la Afrika litafanyika Novemba 16 hadi 23, 2026, jijini Accra, nchini Ghana.

Marion Bosire
2 Min Read

Vanessa Handas, mtetezi wa vijana anatarajiwa kuiwakilisha Kenya katika toleo la tisa la shindano la ulimbwende la Miss Africa Golden.

Shindano hilo maarufu la bara la Afrika litafanyika Novemba 16 hadi 23, 2026, jijini Accra, nchini Ghana.

Miss Africa Golden Pageant linajulikana kwa kuenzi upekee wa watu weusi, urithi wa Afrika na utalii na litawakutanisha washiriki kutoka mataifa 22.

Hivi karibuni, Handas alionekana kwenye vipindi mbali mbali akieleza dhamira yake ya kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya adabu, mwenendo na uanamitindo.

Shindano hilo sasa limeingia katika hatua muhimu ya maandalizi kabla ya washiriki kuwasili, kufuatia uzinduzi wa mfumo wa upigaji kura wa kupima nguvu ya kila nchi itakayoshiriki yaani, “Country Power Voting” jana Oktoba 11, 2026.

Mshiriki atakayepata kura nyingi zaidi kutoka kwa umma atajihakikishia nafasi ya moja kwa moja katika washiriki watatu bora wakati wa fainali kuu itakayofanyika Novemba 23.

Handas kwa sasa anahamasisha mashabiki nchini Kenya kumpigia kura ili apate nafasi hiyo ya moja kwa moja katika washiriki wa fainali.

Mshindi wa jumla atapata safari ya kulipiwa gharama zote ya kuwakilisha Afrika katika shindano la Miss Ocean Africa mwaka 2027 litakalofanyika huko Phuket, nchini Thailand.

Wakenya sasa wanaweza kumpigia Handas kura kupitia mtandao huku akijiandaa kuonyesha utajiri wa utamaduni wa taifa la Kenya.

Share This Article