Watu 139 wafariki baada ya boti kupinduka Djibouti

Manusura walisema ajali hiyo ilitokea karibu na Guhere, katika pwani ya mashariki ya Djibouti.

Marion Bosire
2 Min Read

Angalau watu 139, wakiwemo watoto 15, wamefariki huku wengine 84 wakiripotiwa kutoweka baada ya boti iliyokuwa imebeba wahamiaji kupinduka katika pwani ya Djibouti.

Haya ni kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM.

Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, IOM ilinukuu manusura wakisema ajali hiyo ilitokea karibu na Guhere, katika pwani ya mashariki ya Djibouti, kwenye Ghuba ya Aden karibu na Mlango-Bahari wa Bab al-Mandeb, kati ya Alhamisi usiku na alfajiri ya Ijumaa.

Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Djibouti kuelekea Yemen ikiwa na zaidi ya watu 300. Zaidi ya watu 80, wote wakiwa raia wa Ethiopia, walinusurika ajali hiyo huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea.

Mkuu wa Ujumbe wa IOM nchini Djibouti, Alexandre Coissac, alisema wahudumu wa shirika hilo wako eneo la tukio wakishirikiana na mamlaka za eneo hilo kutoa msaada wa dharura, akielezea masikitiko yake kuhusu vifo hivyo vingi.

Coissac aliambia shirika la habari la Associated Press kuwa idadi hiyo inajumuisha waliozikwa na mamlaka za Djibouti pekee. Wahamiaji wengine walizikwa na wenzao, lakini hawataongezwa kwenye takwimu rasmi hadi mamlaka zithibitishe miili hiyo.

“Janga hili ni ukumbusho wa wazi wa hatari zinazowakabili wahamiaji katika njia hii wanapotafuta fursa za kiuchumi,” aliongeza Coissac.

Mlango-Bahari wa Bab al-Mandeb, ambao una upana wa kilomita 20 katika sehemu yake nyembamba zaidi kati ya Djibouti na Yemen, ni njia inayotumiwa na maelfu ya wahamiaji kutoka Pembe ya Afrika licha ya hatari zake.

Share This Article