Rais wa Marekani Donald Trump amesema Ukraine inafaa kuchagua kiongozi mpya achukue mahala pa Rais Volodymyr Zelenskyy, akimkosoa kwa mashambulizi ya Kyiv dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta nchini Urusi.
Trump anahisi mashambulizi hayo, yamechangia kupanda kwa bei ya dizeli kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani.
“Ninapendekeza wapate kiongozi mpya anayeweza kuafikia makubaliano,” Trump alisema katika Ikulu ya White House Jumamosi, akiongeza kuwa Zelenskyy hafanyi hivyo.
Trump alisema chini ya uongozi wa Zelenskyy, Ukraine imepoteza asilimia 30 ya eneo lake na zaidi ya watu milioni mbili wameuawa katika vita hivyo.
Alisema vita hivyo havikupaswa kuanza na kwamba wakati umefika kwa Ukraine kupata rais mpya.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andriy Sybiga, alimtetea Zelenskyy, akisema anaungwa mkono na wananchi wa Ukraine ambao wana haki ya kuamua mustakabali wa uongozi wao.
Kauli za Trump zimekuja siku moja baada ya kutangaza makubaliano na Rais wa Urusi Vladimir Putin ya kununua dizeli kutoka Urusi ili kupunguza bei ya mafuta nchini Marekani kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula.
Trump amekuwa akimshinikiza Zelenskyy kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Urusi, huku akilaumu Ukraine kwa kupanda kwa bei ya dizeli nchini Marekani badala ya vita vinavyoongozwa na Marekani dhidi ya Iran.
Trump alisema angekuwa rais wa Marekani mwaka 2022, vita kati ya Urusi na Ukraine havingezuka.
“Hakukuwa na sababu ya vita kati ya Ukraine na Urusi kuanza. Vilianza kutokana na uzembe,” alisema.