Ruto ashukuru waliopanda miti siku kuu ya Mazingira

Aliongoza maadhimisho ya Siku ya Mazingira huko Endebess, Kaunti ya Trans Nzoia, jana.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ameshukuru walioshiriki zoezi la kitaifa la upanzi wa miche ya miti lililolenga kupanda miti milioni 5.3 kuadhimisha Siku Kuu ya Mazingira.

Ruto alisema zoezi hilo ambalo ni sehemu ya azma pana ya serikali ya kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032, pia ni juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kurejesha mifumo ya ikolojia iliyoharibiwa.

Katika ujumbe aliochapisha kwenye Facebook, Rais aliwataka Wakenya kuendeleza ari ya upanzi wa miti, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira huko Endebess, Kaunti ya Trans Nzoia, Ruto aligawa miche ya kakao kwa wakulima, hatua iliyoashiria kuanza kwa juhudi za kuanzisha kilimo cha zao hilo nchini Kenya.

Alisema mpango huo unalenga kuhimiza shughuli za upanzi wa miti zinazolinda mazingira na kuwapa wakulima fursa za kujipatia kipato.

Rais pia alizindua teknolojia ya kupanda mbegu kutoka angani ili kukamilisha upanzi wa kawaida na kuharakisha urejeshaji wa misitu iliyoharibiwa.

Aidha, Ruto alizindua Mpango Mkakati wa 2026–2036 wa Mpango Jumuishi wa Uhifadhi wa Mazingira na Uboreshaji wa Maisha ya Jamii katika Mlima Elgon.

Mpango huo unatarajiwa kuongoza juhudi za kurejesha misitu iliyoharibiwa, kulinda rasilimali za maji na kuboresha maisha ya jamii zinazoishi katika maeneo yanayozunguka Mlima Elgon.

Mipango hiyo ni sehemu ya ajenda pana ya serikali ya uhifadhi wa mazingira, inayolenga kuunganisha urejeshaji wa misitu na fursa endelevu za kiuchumi kwa jamii za eneo hilo.

Kupitia upanzi wa miti, fursa mpya za kilimo na teknolojia ya urejeshaji wa misitu, serikali inalenga kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku ikiunga mkono jamii zinazotegemea rasilimali za asili kwa maisha yao.

Share This Article