TEP kubadilishwa jina, kuitwa Linda Mwananchi kuelekea 2027

Hayo yametangazwa leo Ijumaa na kinara wa chama hicho ambaye pia ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.

KBC Digital News
2 Min Read
Edwin Sifuna - Kinara wa TEP ambaye pia ni Seneta wa Nairobi

Chama cha The Equitable Party, TEP kitabadilishwa jina na kuitwa chama cha Linda Mwananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Hayo yametangazwa leo Ijumaa na kinara wa chama hicho ambaye pia ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.

Sifuna amedokeza kuwa Baraza Kuu la TEP limemwandikia barua Msajili wa Vyama vya Kisiasa likimtaka kuwezesha ubadilishaji wa jina hilo.

Amewahakikishia wafuasi wa TEP kwamba hawatatakiwa kujisajili upya kufuatia mabadiliko hayo.

Wakati huohuo, Sifuna pia amepuuzilia mbali uvumi kwamba atajiuzulu wadhifa wake kama Seneta wa Nairobi kufuatia uzinduzi wa chama chake kipya.

Sifuna, aliyechaguliwa kwenye wadhifa huo kwa tiketi ya chama cha ODM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, badala yake anasema atatangaza baadaye ni wakati gani atakihama chama cha chungwa.

Kulingana naye, kama angekuwa hai, kinara wa zamani wa ODM Raila angegombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Raila alifariki Oktoba 15 mwaka jana na chama cha ODM kimetangaza kuwa hakitamsimamisha mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Badala yake, kinasema kitaunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto kuhudumu kwa muhula wa pili na wa mwisho.

Kwa sasa, Sifuna anasema timu yake inafanyia kazi waraka ambao utakuwa msingi wa kutatua masuala yanayoikumba nchi hii katika sekta kama vile uchumi, elimu na afya, miongoni mwa sekta zingine.

Taarifa ya Abdiaziz Hashima na Martin Mwanje

 

Share This Article