Ni kufa kupona huku vyama mbalimbali vya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu vyote vya umma wakikutana leo Alhamisi kubaini hatima ya mgomo wa kitaifa unaoendelea.
Mkutano huo pia utashirikisha maafisa kutoka wizara tofauti katika jitihada za kutafuta suluhu ya haraka ya kumaliza mgomo huo, ambao umesambaratisha masomo katika vyuo vikuu vyote vya umma tangu mapema mwezi huu.
Ukiandaliwa katika makao makuu ya Wizara ya Leba katika jumba la NSSF, mkutano huo unatarajiwa kuangazia pakubwa nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi hao ya mwaka 2025 hadi 2029.
Wahadhiri na wafanyakazi wengine vyuoni wamegoma wakiteta kuhusu nyongeza za awali za mishahara zilizotangazwa na serikali, mazingira duni ya kufanyia kazi na maamuzi yaliyofanywa bila wao kuhusishwa.