Sofiya Nzau atangaza ujio wa ziara yake

Itaanza mwisho wa mwaka huu wa 2026, ikiwa na vituo huko Georgia, Russia na Kyrgyzstan, pamoja na onyesho maalum ndani ya Amsterdam.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Afro-house nchini Kenya Sofiya Nzau, ametangaza rasmi ujio wa ziara yake ya mwaka 2026/27′ itakayopita katika mabara manne.

Ziara hiyo itaanza mwisho wa mwaka huu wa 2026, ikiwa na vituo huko Georgia, Russia na Kyrgyzstan, pamoja na onyesho maalum ndani ya Amsterdam.

Mwimbaji huyo na mtunzi wa nyimbo kutoka Kenya pia atarejea barani Afrika kwa maonyesho yanayotarajiwa kufanyika katika eneo la burudani la Lynk jijini Nairobi tarehe 13 Novemba 2026, na jingine ndani ya Element House jijini Lagos, nchini Nigeria, tarehe 27 Novemba 2026.

Mapema mwaka 2027, ziara hiyo itaelekea Australia, Indonesia, Thailand na New Zealand.

Umaarufu wa Nzau umeongezeka kwa kasi kufuatia wimbo wake wa kimataifa wa “Mwaki”, alioutengeneza pamoja na DJ wa Brazil aitwaye Zerb, ambao umevuka streams milioni 421.

Mnamo 2025, Nzau aliweka historia ya kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kutumbuiza katika tamasha ya “Tomorrowland”. Kwa sasa, anatajwa kuwa msanii anayeongoza kwa usikilizwaji kutoka Afrika Mashariki kwenye Spotify na Apple Music.

Kwa mujibu wa usimamizi wake, tarehe zaidi zitaongezwa kwenye ratiba sambamba na maandalizi ya kutolewa kwa albamu yake ya kwanza ya studio inayosubiriwa kwa hamu.

Share This Article