Idara ya Mahakama na Tume ya Huduma za Mahakama, JSC zilipeleka mchakato wa kushirikisha umma katika kaunti ya Kericho.
Lengo la hatua hiyo ni kupata maoni ya wajumbe wa kamati za watumiaji wa mahakama na wananchi kwa jumla kuhusu bajeti inayopendekezwa ya mwaka 2027/28.
Ujumbe wa Mahakama uliongozwa na Mheshimiwa Jaji Teresa Odera wa Mahakama Kuu ya Kericho na Mheshimiwa Jaji Lynette Omollo wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Kericho.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Msajili wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Rose Makungu, Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama alisisitiza umuhimu wa kushirikisha umma katika sekta ya haki.
Alieleza kuwa haki inayotolewa na Mahakama haiwezi kutimiza madhumuni yake ikiwa haiwezi kuitikia mahitaji ya wananchi wanaokusudiwa kunufaika na huduma hizo.
Msajili Mkuu aliongeza kuwa taarifa zilizokusanywa kutokana na mchakato wa kushirikisha umma awali zimechangia utekelezaji wa mabadiliko yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma.
Mikutano ya kushirikisha umma inayofanyika kote nchini sasa inaelekea Nairobi, ambapo mkutano sawia utaandaliwa katika Mahakama za Dagoretti.