Kampeni zilifungwa rasmi jana nchini Brazil huku raia wa taifa hilo wakitarajia kupiga kura leo kuchagua viongozi wapya.
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva na Seneta wa mrengo wa kulia Flavio Bolsonaro walimaliza kampeni zao hiyo jana, kila mmoja akidhihirisha imani ya kushinda kabla ya raundi ya kwanza ya uchaguzi wa urais unaoonekana kuwa na ushindani mkubwa.
Lula wa miaka 80, alihitimisha kampeni yake ya kutaka kuchaguliwa tena siku ya Jumamosi kwa maandamano yaliyopita katika jiji la Sao Paulo, kitovu cha uchumi wa Brazil, yakivuta umati mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika mkutano wa mwisho wa kampeni.
“Kesho, tutashinda uchaguzi katika raundi ya kwanza,” aliwaambia wafuasi wake, akielezea kura ya Jumapili kama chaguo kati ya “demokrasia na ushenzi” na kuahidi “kushinda mrengo wa kulia uliokithiri”.
Pia ameuonyesha uchaguzi huo kama mtihani wa mamlaka na uhuru wa Brazil, akionya dhidi ya “kuingiliwa” na Washington.
Bolsonaro kwa upande wake aliongoza msafara wa pikipiki kupitia miji kadhaa katika jimbo la Sao Paulo, akifuata mtindo wa kampeni uliotumiwa na babake, kabla ya kufanya mkutano mwingine baadaye huko Rio de Janeiro.
“Nina hakika kwamba kila kitu kipo tayari ili tushinde uchaguzi huu katika raundi ya kwanza,” alisema.
Mwanasiasa huyo wa miaka 45 ni mtoto wa rais wa zamani Jair Bolsonaro, mshirika wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump.