Hatimaye kuna nuru gizani huku Ligi Kuu ya soka nchini Kenya msimu wa mwaka 2026/2027 ikitarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Hii ni baada ya vlabu vya Kariobangi Sharks waliomaliza nafasi ya 16 katika ligi kuu msimu jana na Mombasa United iliyomaliza ya tatu katika ligi ya daraja ya kwanza NSL, kuafikiana kucheza mchujo wa kubaini timu ya mwisho itakayocheza ligini msimu huu.
Yamkini timu hizo mbili zimelegeza misimamo na kukubali kucheza mchujo huo kufuatia upatanisho uliohusisha Shirikisho la Soka nchini, FKF.
Mkondo wa kwanza wa mchujo huo utachezwa Oktoba Mosi katika kaunti ya Mombasa na marudio tarehe 6 mwezi ujao jijini Nairobi.
Utata baina ya timu hizo mbili kupitia kesi mahakamani umechelewesha kuanza kwa msimu wa mwaka 2026/2027 wa Ligi Kuu kwa takriban mwezi mmoja.