Wanamuziki wa Tanzania Harmonize na Nandy pamoja na wenzao wawili, wameadhibiwa na Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA kutokana na sababu mbali mbali.
Harmonize analaumiwa na BASATA kutokana na wimbo wake uitwao, “Kudos” ambao unasemekana kutokidhi mahitaji ya maadili ya Tanzania.
Katika kumwadhibu msanii huyo BASATA imemwagiza aondoe video ya wimbo huo kwenye majukwaa yote ya mitandao nchini Tanzania na alipe faini ya shilingi milioni 5 pesa za Tanzania atika muda wa siku 14.
Mwanamuziki huyo haruhusiwi kujihusisha na shughuli za sanaa hadi pale ambapo atatimiza masharti hayo.
Mwelekezi wa video hiyo, Kennedy Sanga, naye amechukuliwa hatua zinazofanana, ikiwemo kusitishiwa kujishughulisha na shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa na BASATA.
Nandy, alijipata matatani na BASATA kutokana na vazi alilovaa jukwaani katika fainali ya Miss Universe 2026.
Nandy alikiri kosa, akaondoa video hiyo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na tayari amelipa faini ya shilingi milioni tatu, na ameruhusiwa kuendelea na shughuli za sanaa chini ya uangalizi wa BASATA.
Mwandaaji wa Miss Universe Tanzania naye amechukuliwa hatua kwa kumruhusu Nandy kutumbuiza akiwa amevaa mavazi hayo.
Haya yanajiri wakati anaandaa tamasha yake ya Dar es Salaam tarehe 26 mwezi huu wa Septemba.
Mwingine ambaye ameadhibiwa na BASATA ni mwandaaji wa mashindano ya urembo ya Miss Grand Tanzania anayelaumiwa kwa kuendesha mashindano hayo bila kibali cha BASATA.
Millen Magese ameagizwa kulipa faini ya shilingi milioni tatu na kutojihusisha na shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa.