Uhusiano kati ya wanamuziki wa Kenya Otile Brown na Jovial unaonekana kuendelea kuzorota hata zaidi, huku Otile akisema hataki Jovial ahudhurie mazishi yake.
Akizungumza katika mahojiano mtandaoni leo Septemba 23, 2026, Otile Brown alitoa kauli hii inayoonyesha mfarakano mkubwa na ambao haujasuluhishwa kati ya wasanii hao wawili.
Mzozo kati ya wawili hao ulianza wazi Julai 2026 wakati wa mahojiano kwenye kituo cha runinga, ambapo Jovial aliibua malalamiko kuhusu mrabaha ambao haukulipwa.
Alidai kukumbana na changamoto za kifedha wakati nyimbo zao za pamoja zilizovuma, kama “Such Kinda Love” na “Jeraha”, zilipokuwa zikiongoza kwenye chati za muziki.
Alisema kuwa malipo yalikuwa tatizo kubwa na kueleza kuwa aliwahi kulala kwenye sakafu huko Mirema licha ya mafanikio ya muziki wao.
Otile Brown alijibu madai hayo akitetea uongozi wake na kuonyesha kuwepo kwa changamoto za kimfumo katika sekta ya utoaji na usambazaji wa muziki kanda hii.
Alisisitiza kuwa mara kwa mara alikuwa akimsaidia Jovial kifedha kutoka mfukoni mwake pindi pesa zilipopatikana.
Otile anasema amekuwa akimsaidia Jovial katika nyakati ngumu za maisha, kama kulipa bili zake za hospitali wakati wa kujifungua kisha akamgeuka na kudai yeye ndiye baba mtoto.
Uchunguzi wa DNA baadaye ulimwondolea dai hilo.
Jovial aliomba msamaha kwa umma kupitia mitandao ya kijamii, akionyesha majuto lakini kauli za hivi karibuni za Otile Brown zinaonyesha kuwa msamaha huo haukurekebisha uhusiano wao.