Waandaaji wa tamasha ya kitamaduni ya jamii ya Wanubi almaarufu Sabala Festival, wametangaza rasmi tarehe ya awamu ya 20 ya hafla hiyo.
Katika tangazo kwenye akaunti za mitandao ya kijamii za tamasha hiyo, waandalizi walisema hafla ya mwaka huu itaandaliwa Novemba 27 hadi 30, 2026.
Sherehe hii kubwa ya utamaduni inarejea kihistoria jijini Nairobi, Kenya, huku hafla kuu ya gala ikianza Ijumaa, Novemba 28, 2026, katika Hoteli maarufu ya Hilton.
Kwa miongo miwili, tamasha hii imekuwa jukwaa muhimu la kuonyesha urithi tajiri, fahari hai na mila mbalimbali za utamaduni wa Wanubi kote Afrika Mashariki.
Msisimko unaoambatana na maandalizi ya tamasha ya mwaka huu unaonekana wazi. Kabla ya hafla kuu, shughuli mbalimbali za kijamii tayari zinaendelea katika maeneo tofauti ya Nairobi.
Matukio haya yenye hamasa yanaongozwa na Malkia mpya wa Utamaduni wa 2026, Bi. Mariam Abdulmagid, ambaye anaongoza juhudi za kushirikisha vijana na wazee kwa pamoja.
Ili kuwasaidia washiriki wa kimataifa na wa kikanda wanaosafiri kwa ajili ya maadhimisho haya, kampuni ya usafiri wa angani nchini, Kenya Airways imeshirikiana na waandaaji wa tamasha.
Shirika hilo linatoa punguzo la hadi asilimia 12 kwa safari za ndege kuelekea Nairobi kati ya Novemba 20 na Desemba 7, 2026, huku waashiriki wakihimizwa kuhifadhi nafasi mapema ili kushiriki katika sherehe hii ya kihistoria ya siku nne ya kuadhimisha urithi.