Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika Patrice Motsepe anatarajiwa kufanya ukaguzi wa viwanja vya Kenya leo kwa maandalizi ya kipute cha mataifa ya Afrika, AFCON mwaka ujao.
Motsepe alitua Nairobi Alhamisi usiku akitokea Dar es Salaam, Tanzania ambapo pia aliakagua uwanja wa kitaifa wa Benjamin Mkapa.
Ziara ya Motsepe ni ya hivi punde huku ikisalia miezi tisa pekee kabla ya kuanza kwa kindumbwendumbwe hicho kinachoandaliwa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza.
Kenya inashirikiana na majirani Tanzania na Uganda kuandaa patashika hiyo ya 36, kati ya mwezi Juni na Julai mwaka ujao.
Uwanja wa Kasarani unakarabatiwa tayari kwa kipute hicho huku ule wa Talanta ukiwa takriban asilimia 90 kukamilika.