Rais William Ruto aliendelea na ziara yake katika eneo la Nyanza, wakati huu akielekea katika kaunti ya Migori ambako alikagua na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ruto akitembelea kituo cha Sibuoche katika eneo bunge la Uriri ambako aliwasihi wakazi kuunga mkono serikali jumuishi.

Miongoni mwa miradi aliyozindua ni ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 32 ya Kanyawanga-Kwoyo-Madiaba-Dede-Odongo Oher-Rapogi-Awendo.
Ruto alisema ujenzi wa barabara hiyo kwa kima cha shilingi bilioni 2.25 utaboresha uunganishaji, kurahisisha usafiri na kupanua masoko na upatikanaji wa huduma muhimu.

Ni wakati huo ambapo kiongozi wa taifa alizidi kuushambua upinzani akiutaja kuwa muungano usiokuwa na uongozi, ajenda wala mpango wowote wa kulinufaisha taifa.
“Hatuwezi tukacheza kamari na mustakabali wa nchi na watu ambao hawana ajenda, mpango wala maono,” alisema Rais Ruto.
Viongozi wa eneo hilo, wakiongozwa na Gavana Ochilo Ayacko, walimshabikia Rais Ruto wakimsifu kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, masoko na usambazaji wa umeme na maji kwa wakazi.
Rais Ruto amekuwa akizuru maeneo mbalimbali nchini wakati akizindua miradi ya maendeleo na kunadi serikali ya Kenya Kwanza takriban mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Ruto ameahidi kuubwaga upinzani kwenye uchaguzi huo wakati akitafuta kuongoza nchi kwa muhula wa pili.