Wanyama 50 wafariki kutokana na kimeta nchini Zambia

Watu kadhaa pia wameambukizwa ugonjwa huo, baada ya kudaiwa kula wanyamapori ambao wameambukizwa kimeta katika eneo la Mto Munyamadzi.

Tom Mathinji
1 Min Read
Wanyamapori 50 wafariki kutokana na kimeta au Anthrax nchini Zambia.

Maafisa wa serikali nchini Zambia wamewaonya wakazi dhidi ya kula au kusambaza nyama kutoka kwa wanyamapori, baada ya kuzuka kwa ugonjwa wa kimeta au Anthrax.

Idara ya kitaifa ya kukabiliana na majanga nchini humo, imesema baadhi ya wanyamapori walioambukizwa kimeta ni pamoja na Kiboko 46, Tembo 8, Mamba mmoja, na Nyati 5, ambao wameripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo.

Kulingana na maafisa nchini humo, watu kadhaa pia wameambukizwa ugonjwa huo, baada ya kudaiwa kula wanyamapori ambao wameambukizwa kimeta katika eneo la Mto Munyamadzi.

Aidha, idara hiyo imetoa wito kwa wananchi kuripoti visa vyovyote vinavyoshukiwa kuwa vya ugonjwa wa kimeta, katika juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, huku shughuli za uwindaji wanyamapori zikisitishwa hadi ugojwa huo utakapodhibitiwa.

Wakati huo huo, wananchi wameonywa dhidi ya kuwachinja wanyama ambao tayari wamefariki, ili kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa kimeta.

Si mara ya kwanza kwa Zambia kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kimeta, mwaka 2023, watu wanne walifariki kutokana na ugonjwa huo, kwenye mlipuko wa kimeta uliotajwa kuwa mkubwa zaidi.

Kimeta ni ugonjwa kuambukiza ambao husababishwa na bakteria unaowaathiri wanyama na pia huambukizwa binadamu.

Share This Article