Rais William Ruto amewaonya wanasiasa wanaozua vurumai nchini akisisitiza kuwa kamwe siasa za uchochezi na vurugu hazina nafasi katika taifa la Kenya.
Akizungumza leo Jumatatu katika mkutano wa kisiasa kaunti ya Kisumu, Ruto alisema lengo lake ni kueneza amani, kuleta uthabiti na umoja humu nchini pamoja na kukabiliana na dondasugu la ukabila.
Aidha, Rais alikariri kujitolea kwa serikali kuimarisha uchumi wa nchi na kumaliza umaskini.
Aliongezea kuwa kama njia ya kumaliza uhaba wa makazi kwa maafisa wa polisi, serikali yake imejenga nyumba 20,000 kote nchini ili kuhakikisha wanaishi katika mazingira nadhifu.
Akiwa kaunti ya Kisumu, Rais alifungua makao makuu ya kituo cha maafisa wa polisi eneo la Kisumu magharibi.
Alisema serikali imewekeza shilingi bilioni 44 chini ya mpango wa nyumba za gharama nafuu kwa kujenga nyumba 12,000, masoko 20 na vyumba vya mabweni ya wanafunzi vilivyo na vitanda 12,000.
Ruto alianza ziara ya Nyanza siku ya Jumapili akitarajiwa kuzuru kaunti za Kisumu, Migiori, Homa Bay na Siaya.