A Pass awaza kubadili eneo la tamasha yake ijayo

Alitaja kutokuwa na uhakika kuhusu upatikanaji wa uwanja anaopendelea wa Kololo.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Uganda, A Pass, anafikiria upya mipango yake ya kufanya tamasha yake ya moja kwa moja katika uwanja wa ndege wa Kololo mwakani, akitaja kutokuwa na uhakika kuhusu upatikanaji wa ukumbi huo.

Mwezi uliopita, A Pass alitangaza mipango ya kufanya tamasha ya moja kwa moja na kutaja Kololo Airstrip kama eneo analopendelea la maandalizi ya tukio hilo.

Hata hivyo, akiwa mubashara kwenye mtandao wa TikTok Alhamisi usiku, mwimbaji huyo alisema bado anafikiria kuhusu ukumbi huo na huenda akatafuta chaguo jingine.

“Nataka kulifanya Kololo lakini tatizo pekee la Kololo ni kwamba watu wa huko hawatabiriki. Wakati mwingine mtu anaandaa tamasha huko, halafu unasikia wanaenda kufanya sherehe fulani. Kwa hiyo wakati mwingine sitaki kutokuwa na uhakika,” alisema A Pass.

Kwa mujibu wa mwimbaji huyo, hali hiyo ya kutokuwa na uhakika kuhusu Kololo inamlazimisha kuzingatia kumbi nyingine ambazo zitampa uhakika zaidi kwamba tamasha hiyo itafanyika kama ilivyopangwa.

Alitaja Uwanja wa Namboole kama mojawapo ya maeneo yanayoweza kutumika, lakini akakiri kuwa viwanja pia vina changamoto zake, hasa kuhusu mfumo wa sauti.

“Labda tufanye Namboole? Lakini si watatusumbua? Viwanja si rahisi sana na vina changamoto kidogo kuhusu sauti, lakini najua lolote linawezekana. Ningependa Kololo, lakini kuna kutokuwa na uhakika,” aliwaza.

A Pass bado hajatangaza ukumbi wa mwisho wa tamasha hilo, huku mashabiki wakisubiri taarifa zaidi kuhusu tamasha lililopangwa kufanyika mwakani.

Share This Article