Polisi walaani ghasia katika mkutano wa Naibu Rais Embu

Uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kikamilifu mazingira yaliyosababisha tukio hilo na kuwabaini wote waliohusika.

Marion Bosire
1 Min Read

Huduma ya Kitaifa ya Polisi, NPS, imewalaani vikali waliohusika katika tukio la vurugu lililotokea huko Nembure, Kaunti ya Embu, ambapo kundi la watu linadaiwa kujaribu kuvamia mkutano wa hadhara ulioongozwa na Naibu Rais Kithure Kindiki.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Septemba 12, 2026, polisi walisema maafisa walichukua hatua madhubuti baada ya kundi hilo kujaribu kuingia katika mkutano huo kinyume cha sheria, na kuwazuia washambuliaji hao huku wakirejesha utulivu.

Washukiwa kadhaa walikamatwa katika eneo la tukio baada ya makabiliano hayo.

Hata hivyo, tukio hilo lilisababisha mtu mmoja kujeruhiwa vibaya na baadaye kufariki, huku magari sita yakichomwa moto na watu wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye vurugu hizo.

Huduma ya Kitaifa ya Polisi ilisema uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kikamilifu mazingira yaliyosababisha tukio hilo na kuwabaini wote waliohusika.

Polisi wameonya kuwa mtu yeyote atakayebainika kushiriki vurugu hizo au vitendo kama hivyo vya kuvunja sheria atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Huduma hiyo imesema hakutakuwa na msamaha kwa yeyote, ikisisitiza kuwa itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kudumisha sheria na utulivu na kulinda maisha na mali kote nchini.

Aidha, polisi wamewahakikishia wananchi kuwa taarifa zaidi zitatolewa kadiri uchunguzi unavyoendelea na pale ambapo itakuwa salama kufanya hivyo.

Share This Article