Amodei ahimiza kupunguzwa kwa kasi ya ustawishaji AI

Pendekezo lake linataka kuwepo kwa ufuatiliaji huru wa mifumo ya AI wakati inatengenezwa.

Marion Bosire
2 Min Read
Dario Amodei, Mkurugenzi Mkuu kampuni ya Anthropic

Mkuu wa kampuni ya Akili Unde, AI, iitwayo Anthropic Dario Amodei, ametowa wito wa kupunguzwa kwa kasi ya ustawishaji wa Akili Unde huku hofu ya kutoweka kwa binadamu ikitanda.

Hili ndilo onyo la hivi punde zaidi la mtaalamu wa maswala ya AI katika mashindano ya kutengeneza mifumo yenye nguvu zaidi ya AI, huku Amodei akitaka sekta hiyo kupunguza kasi ya maendeleo na kuimarisha ukaguzi wa usalama.

Katika makala yenye kichwa “We Must Pace the Frontier”, Amodei alisema maendeleo ya AI yanapaswa kuendelea, lakini akaonya kuwa hatari zinazohusishwa na teknolojia hiyo ni kubwa, akisema serikali na kampuni zinahitaji muda wa kushughulikia vitisho vinavyoweza kujitokeza.

Pendekezo lake linataka kuwepo kwa ufuatiliaji huru wa mifumo ya AI wakati inatengenezwa, kanuni za usalama zinazotumika katika sekta nzima na usimamizi wa kimataifa.

Wito huo umeungwa mkono na wapinzani wake, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa OpenAI, Sam Altman, pamoja na Elon Musk. Altman alisema anakubaliana kuwa maendeleo ya AI yanahitaji kudhibitiwa na akataja tathmini huru kuwa wazo zuri.

Hofu imeongezeka kufuatia maonyo ya mtafiti wa zamani wa Anthropic, Jacob Coxon, aliyesema baadhi ya wafanyakazi wa AI wana wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa binadamu.

Licha ya maonyo hayo, Rais wa Marekani Donald Trump amepinga wito wa kupunguza kasi, akisisitiza kuwa Marekani lazima ishinde katika mashindano ya AI.

Share This Article