Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ametetea agizo la Rais William Ruto kwa wafanyabiashara wa kigeni kuhalalisha uwepo wao nchini Kenya, akidokeza kuwa agizo hilo linambatana na sheria na linalinda fursa zilizopo kwa wafanyabiashara wa hapa nchini.
Kulingana na Wetang’ula, Kenya iko wazi kwa wawekezaji na raia wengine wa kigeni, lakini akasisitiza kuwa wanaofanya biashara hapa nchini Kenya ni sharti wawe na leseni na vibali vingine.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwawezesha wahudumu wa bodaboda katika eneo bunge la Endebess, kaunti ya Trans Nzoia, Wetang’ula alisema matamshi ya Rais hayapaswi kutafsiriwa kama hatua ya kufunga milango ya Kenya kwa raia wengine wa Afrika.
Spika huyo alidokeza kuwa Kenya imeendelea kuwakaribisha wageni na wawekezaji kutoka mataifa mengine ya Afrika, ikiwa ni pamoja na wale wa kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Kile ambacho Rais anataka na sisi sote tunataka, ni kwamba ukiingia nchini Uganda, ni sharti ujisajili kwa utawala wa nchi hiyo ili wafahamu kuna mgeni ameingia katika taifa lao,” alidokeza Spika Wetang’ula.
Alisema hatua hiyo inapaswa kutekelezwa wakati raia wa Afrika Mashariki wanapoingia Kenya, akidokeza kuwa taifa hili linapaswa kufahamu ni nani ameingia na kwa lengo gani.
Matamshi ya Wetang’ula yanajiri huku hisia mbali mbali zikiibuliwa kufuatia agizo la Rais kwamba raia wote wa kigeni wanaofanya biashara nchini Kenya kuhakikisha wanaleseni na vibali vya kuwa hapa nchini.