Serikali imo mbioni kuanzisha Kituo cha Kitaifa cha Mawasiliano (NCC) kitakachotumiwa kama kituo kikuu cha kuhifadhi taarifa za serikali.
Katibu katika Idara ya Utangazaji na Mawasiliano Stephen Isaboke anasema serikali pia imeazimia kutumia mfumo wa dijitali kueneza taarifa zake kwa umma ili kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia watu wengi haraka iwezekanavyo.
“Mawasiliano ya serikali yatatumia ipasavyo sera ya dijitali kwanza, yakiacha nafasi ndogo ya kufasiriwa visivyo,” alisema Isaboke wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Good Morning Kenya katika runinga ya KBC Channel1.
“Sera ya mawasiliano itahakikisha uelezeaji endelevu wa mambo yalivyo, takwimu, na ushahidi,” aliongeza wakati akizungumzia mada ya mawasiliano ya serikali katika enzi ya dijitali.
Huku akielezea kuwa ufadhili wa kutosha utatolewa kwa mawasiliano ya serikali kuanzia sasa, Isaboke pia aliongeza kuwa mawasiliano na ushiriki wa umma sasa ni muhimu zaidi kwa kila mradi wa serikali.
Kulingana naye, licha ya serikali ya Rais William Ruto kufanya mengi tangu kuingia madarakani, kumekuwa na tatizo la mawasiliano ambalo limefanya miradi mingi kutoangaziwa ipasavyo machoni pa umma, pengo aliloahidi kuwa litazibwa hivi karibuni.
Awali, kwenye taarifa, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei alizitaka idara mbalimbali za serikali kuwa mstari wa mbele katika kunadi miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Koskei akilalama kuwa kushindwa kufanya hivyo kumesababisha umma kutokuwa na ufahamu wa miradi mingi ya kuufahidi inayotelezwa na serikali.