Madeni mwiba kwa serikali kuu na za kaunti, alalama Ruto

Rais amesifia ushirikiano ulioimarika kati ya serikali kuu na serikali za kaunti akisema umesaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwa kiwango kikubwa nchini.

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameelezea mashaka kuhusu madeni zinazodaiwa serikali kuu na za kaunti kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Ruto sasa ameiagiza Ofisi ya Mdhibiti wa Bajeti na ile ya Mkaguzi Mkuu kuingilia kati ili kuthibitisha madeni zinazodaiwa serikali hizo kwa lengo la kutolemaza shughuli za wafanyabiashara wanaozidai serikali hizo madeni halali.

“Huku uchaguzi mkuu unapokaribia, madeni yanasalia suala linaoibua wasiwasi katika ngazi zote za serikali. Yanaathiri biashara, kuharibu kazi, na kudhoofisha imani katika serikali,” alilalama Rais Ruto.

“Kwa biashara nyingi, hasa biashara ndogo ndogo na za kadri, madeni ambayo hayajalipwa ya serikali siyo tu suala la uhasibu. Ni mtaji uliozuiliwa, mishahara iliyocheleweshwa na vyanzo vya mapato vilivyo hatarini.”

Ni hali ambayo imemfanya kiongozi wa nchi kuitaka Ofisi ya Mdhibiti wa Bajeti na ile ya Mkaguzi Mkuu wa serikali kuingilia kati ili kubaini madeni halali kwa lengo la kuhakikisha wanayoyadai wanalipwa ili kuwawezesha kuendelea na biashara zao.

Ruto aliyasema hayo alipoongoza mkutano wa uratibu wa serikali kuu na zile za kaunti uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.

Ni wakati huo ambapo alisifia ushirikiano ulioimarika kwa kiwango kikubwa kati ya serikali kuu na zile za kaunti.

Kupitia ushirikiano huo, alisema serikali za kaunti zimeweza kuboresha utoaji huduma za matibabu chini ya mageuzi ya Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA, kupanua mitungo thamani ya kilimo, kuharakisha ustawi wa viwanda vya uzalishaji na kukumbatia mifumo ya dijitali ambayo inafanya utunzaji rekodi, uwekaji mipango na ukusanyaji mapato kuwa wa kisasa.

“Mafanikio haya yanaashiria ukweli ambao ni wepesi lakini muhimu, kwamba wakati serikali kuu na za kaunti zinapofanya kazi pamoja, Wakenya hupata huduma bora, rasilimali za umma hutoa thamani bora na nchi yetu kusonga mbele haraka,” aliongeza Rais Ruto.

 

 

 

 

 

Share This Article