Serikali imedumisha uwazi kwenye Mswada wa Fedha 2026, asema Mwaura

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura,  amewasuta wakosoaji kwa kueneza habari za uwongo kuhusu mswaada wa Fedha.

Tom Mathinji
2 Min Read
Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura.

Serikali imepuzilia mbali madai yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Mswaada wa Fedha 2026, ikiyataja kuwa uvumi usio na msingi na yaliyochochewa kisiasa.

Akizungumza na wanahabari leo Jumatano, Msemaji wa serikali Isaac Mwaura,  aliwasuta wakosoaji kwa kueneza habari za uwongo kuhusu mswaada huo akisema madai hayo aliyodokeza kuwa yanazua hofu miongoni mwa wakenya.

Mwaura alitoa wito kwa wananchi kuusoma mswada huo wenyewe badala ya kutegemea majadiliano potovu yanayosambazwa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu mswada huo.

Baadhi ya madai yaliyotupiliwa mbali na serikali kuhusu Mswada wa Fedha ni ushuru mpya kwa nguo kuukuu almaarufu Mitumba, nyongeza ya ushuru kwa mapato kutoka kwa nyumba za kukodisha, na ushuru mpya kwa simu za rununu na malipo kupitia mtandaoni.

Kulingana na Mwaura, baadhi ya mapendekezo yaliyokumbwa na utata hapo awali, yaliondolewa au kufanyiwa marekebisho kabla ya kuchapishwa kwa Mswada huo na Hazina Kuu.

Alifafanua kwamba pendekezo la kuongeza ushuru unaotokana na mapato ya nyumba za kukodisha kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 10 liliondolewa, pamoja na pendekezo la ushuru kwa nguo za mitumba.

Alipongeza Mswada huo akisema umechukua hatua za kuwakinga wakenya dhidi ya hali ya sasa ya kiuchumi hasaa kwa kupunguza ushuru kwa bidhaa za nyumbani, huku ukipiga jeki sekta muhimu za kiuchumi.

TAGGED:
Share This Article