KECOBO yaalika maombi ya leseni za CMOs kwa mwaka 2027

Waombaji wanashauriwa kupitia tangazo kamili la umma na kuhakikisha maombi yao yanakidhi mahitaji yote .

Marion Bosire
1 Min Read

Bodi ya Hakimiliki ya Kenya, KECOBO, imealika mashirika yanayotimiza vigezo kuwasilisha maombi ya leseni za kuwa Mashirika ya Usimamizi wa Haki kwa Pamoja yaani ‘Collective Management Organisations, CMOs’ kwa mwaka 2027.

Mchakato huo wa utoaji leseni ni sehemu ya jukumu la KECOBO la kudhibiti na kusimamia mashirika hayo yanayohusika na usimamizi wa hakimiliki na haki zinazohusiana kwa niaba ya wabunifu, wasanii na wamiliki wengine wa haki.

Mashirika yanayovutiwa yanatakiwa kuwasilisha maombi yao kupitia mfumo wa E-Citizen kufikia Septemba 18, 2026, saa 11:00 jioni.

Waombaji wanashauriwa kupitia tangazo kamili la umma na kuhakikisha kuwa maombi yao yanakidhi mahitaji yote yaliyowekwa chini ya Sheria ya Hakimiliki na Kanuni za Hakimiliki (Usimamizi wa Pamoja) ya mwaka 2020.

Kwa sasa, kuna mashirika manne ya usimamizi wa haki kwa pamoja chini ya KECOBO ambayo ni Shirika la Hakimiliki za Muziki Nchini Kenya, MCSK na Chama cha Watayarishaji muziki Nchini Kenya, KAMP.

Mengine ni Chama cha Haki za Watumbuizaji Nchini Kenya, PRISK na Chama cha Haki za Utoaji Nakala, KOPIKEN.

Leseni za CMOs hudumu mwaka mmoja na mashirika yanapaswa kutuma maombi miezi mitatu kabla ya mwisho wa muda wa leseni iliyopo.

Share This Article