Rais William Ruto ametuma risala za rambirambi kufuatia kifo cha mumewe Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Hafidh Ameir Hassan.
Hafidh alifariki mapema leo Jumatatu wakati akitibiwa ugonjwa wa moyo.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Hafidh Ameir Hassan, mumewe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Rais Ruto kwenye ujumbe wake wa maombolezo.
“Kwa niaba ya Serikali na watu wa Kenya, Mama Taifa, familia yangu na kwa niaba yangu, natuma risala za rambirambi kwa Rais Samia, familia yake na watu wa Tanzania. Rais Samia amepoteza mwenza wake wa maisha, watoto wake baba yao mpendwa, na Tanzania raia wake mahiri.”
Akitangaza kifo hicho, Makamu mpya wa Rais wa nchi hiyo Deogratius Ndejembi alisema Hafidh alifariki wakati akipokea matibabu katika hospitali ya kumbukumbu ya Emilio Mzena visiwani Zanzibar.
“Ndugu wananchi, kwa masikitiko makubwa, nawajulisha taarifa ya kifo cha Mhemimiwa Hafidh Ameir Hassan, mume wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kilichotokea leo, tarehe 7, Septemba 2026 majira ya saa mbili asubuhi katika hpsitali ya kumbukumbu ya Emilio Mzena Zanzibar alipokuw akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo,” alitangaza Ndejembi.
Mipango ya mazishi inaendelea.