Afrika Kusini yaibuka kidedea Afrika mashindano ya ulimbwende

Mwakilishi wa Kenya Trizah Muhenje Akala, aliondolewa katika hatua ya robo fainali ya 40 bora ya mashindano ya Miss World.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwakilishi wa Afrika Kusini, Romanda Hombir, ametawazwa ‘Miss World Africa 2026’ baada ya kufanya vyema katika fainali kuu ya 73 ya mashindano ya ulimbwende ya Miss World huko Nha Trang, Vietnam.

Hombir alivutia majaji kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuwa mshiriki wa Kiafrika aliyefanya vizuri zaidi, baada ya kufuzu hadi kiwango cha 6 bora kwenye mashindano hayo ya kifahari.

Safari yake kuelekea hatua ya mwisho ilianza kwa mafanikio mapema, aliposhinda raundi ya bara ya ‘Head-to-Head Challenge’.

Katika raundi hiyo, alifanya vizuri dhidi ya wawakilishi mahiri kutoka Nigeria, Kenya, Zambia na Eritrea, na hivyo kupata moja kwa moja nafasi katika walimbwende 40 wa dunia.

Mbali na uzuri na umaridadi wake, Hombir alitumia jukwaa hilo la kimataifa kuendeleza kazi yake muhimu ya utetezi wa masuala ya afya ya wanawake kama ‘endometriosis’, ‘PCOS’ na ‘fibroids’.

Katika fainali hiyo kuu ya Miss World 2026 iliyofanyika Septemba 5, 2026, wawakilishi kutoka Afrika Mashariki waliondolewa katika hatua tofauti za mashindano.

Mwakilishi wa Kenya, Trizah Muhenje Akala, aliondolewa katika hatua ya robo fainali ya 40 bora. Kabla ya kuondolewa, alifanikiwa kufuzu kama mmoja wa washiriki wa bara katika mashindano ya ujuzi wa teknolijia ya mawasiliano na urembo wenye kusudi.

Latricia Ian Sawe wa Tanzania, pia aliondolewa katika hatua ya robo fainali ya 40 bora. Alifanya vyema katika hatua za awali za mashindano na kuwa mmoja wa washiriki wa bara waliofuzu katika mashindano ya ujuzi wa teknolijia ya mawasiliano.

Mwakilishi wa Uganda Trivia Elle Muhoza, aliondolewa kabla ya mchujo wa robo fainali, na hivyo kukosa nafasi ya kuingia awamu ya 40 bora.

Share This Article