Nyota wa muziki nchini Uganda, Jose Chameleone, kwa mara nyingine ameonyesha hadharani upendo wake mkubwa kwa mamake, Prossy Mayanja.
Alimtakia heri ya siku ya kuzaliwa kupitia ujumbe wa hisia aliochapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Mwimbaji huyo wa kibao “Valu Valu” alichapisha picha ya awali ya Mama Prossy akiwa msichana na kuandika, “Happy Birthday mpenzi wangu, Mama yangu! Kipenzi changu, Shujaa wangu. My bestie Prossy!!! Maaama Nkwagala nnyo, nnyo, nnyo.”
Ujumbe huo wa hisia, ambao umechanganya Kiingereza, Kiswahili na Luganda, ni ushahidi mwingine wa hadharani unaoonyesha uhusiano wa karibu uliopo kati ya Chameleone na mama yake.
Chameleone amekuwa akitumia nyakati mbalimbali kumsherehekea na kumthamini Mama Prossy lakini je ni kwa nini?
Mama Prossy amekuwa akionekana kuwa mtu wa karibu sana kwa mwimbaji huyo hata anapokuwa katika nyakati ngumu.
Ikumbukwe kwamba alipoanza kuugua picha zilizosambaa mitandaoni kwa mara ya kwanza zilimwonyesha mamame akiwa kando ya kitanda chake hospitalini akimuuguza.
Wakati mwingine msanii huyo alidhihirisha upendo kwa mamake ni wakati alisafiri naye hadi Dar es Salaam kabla ya hafla kubwa ya Bongo Flava Honors, akieleza kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kuzuru Tanzania.
Kwa kuwa yeye mwenyewe alikuwa akielekea nchini humo kwa ajili ya kuheshimiwa, aliamua kuhakikisha mamake anakuwa pembeni yake katika wakati huo muhimu.