Mabingwa wa Dunia Emmanuel Wanyonyi na Faith Cherotich, na Doris Lemngole ni Wakenya watatu watakaokuwa uwanjani Ijumaa usiku katika siku ya kwanza ya mkondo wa mwisho wa Diamond League mjini Brussels nchini Ubelgiji.
Wanyonyi ambaye anaongoza msimamo, atatimka mbio za mita 800 akipambana na Djamel Sedjaati wa Algeria na Gabriel Tual wa Ufaransa.
Fainali hiyo itang’oa nanga saa tatu na dakika 42 usiku.
Cherotich kwa upande wake atashirikiana na mwenzake Doris Lemngole kumenyana na mpinzani wa jadi Winfred Yavi kutoka Bahrain na bingwa wa zamani wa Olimpiki Peruth Chemutai wa Uganda kuanzia saa tatu na dakika 23.
Washindi wa mbio hizo watapokea shilingi milioni 7.8 kila mmoja na kufuzu kwa mashindano ya Ultimate baadaye mwezi ujao.