Wanafunzi wa Vyuo Vikuu, TVET waongezwa muda wa kuomba ufadhili

Wanafunzi walioongezewa muda ni wale wanaotuma maombi ya ufadhili kwa mara ya kwanza. Wana hadi Septemba 21 mwaka huu kutuma maombi.

Martin Mwanje
1 Min Read
Julius Ogamba - Waziri wa Elimu

Wanafunzi Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kiufundi, TVET wanaotuma maombi ya ufadhili kwa mara ya kwanza wana kila sababu ya kutabasamu baada ya muda wa kutuma maombi kuongezwa hadi Sptemba 21 mwaka huu. 

Makataa ya kutuma maombi kwa wanafunzi hao yalikuwa Agosti 31.

Kwenye taarifa, Waziri wa Elimu Julius Ogamba ameagiza Mfuko wa Vyuo Vikuu na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) kuongeza muda huo ili wanafunzi waliokosa kuzingatia makataa ya awali wapate fursa ya kutuma maombi ya ufadhili.

“Wanafunzi wote wanaostahiki wanaotuma maombi kwa mara ya kwanza katika Vyuo Vikuu na TVET wanaombwa kutuma maombi haraka ndani ya muda ulioongezwa,” alisema Waziri Ogamba kwenye taarifa.

“Ili kufutilia mbali mashaka yoyote, umma unataarifiwa kwamba maombi ya ufadhili kwa mara ya kwanza yatazingatiwa na kutayarishwa kwa mujibu wa Mfumo wa Sasa wa Ufadhili unaotoa Kipaumbele kwa Wanafunzi.”

Hadi kufikia sasa, wanafunzi 789,422 wametuma maombi ya ufadhili huku serikali ikitoa ufadhili wa shilingi bilioni 22.12 katika muhula wa kwanza.

 

 

Share This Article