Katz akiri Israel inataka kuondoa Wapalestina Gaza

Anasema Rais Trump amesitisha tu kwa muda mpango ambao watetezi wa haki za binadamu wanasema unalenga kusafisha eneo hilo kikabila.

Marion Bosire
2 Min Read

Israel bado inaendeleza juhudi za kuondoa Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amekiri.

Katz anasema Rais wa Marekani Donald Trump amesitisha tu kwa muda mpango ambao watetezi wa haki za binadamu wanasema unalenga kusafisha eneo hilo kikabila.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na chapisho la Israel la Ynet Jumatano, Katz alisema kupunguza idadi ya watu Gaza bado ni suluhisho pekee.

“Mwishowe, hakuna suluhisho la kweli kwa Gaza bila uhamaji huu,” Katz alisema, kwa mujibu wa Times of Israel.

Watetezi wa haki za Wapalestina wamekuwa wakidai kwa karibu miaka mitatu kwamba lengo kuu la vita vya Israel dhidi ya Gaza, ambavyo wameviita vya mauaji ya kimbari, ni kulisafisha eneo hilo la Palestina kikabila.

Baadhi ya maafisa wa Israel wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia hapo awali wamezungumza waziwazi kuhusu kuwapunguza Wapalestina Gaza.

Rais Trump aliunga mkono wazo hilo mapema katika kipindi chake cha urais, akisema Marekani ingeichukua eneo hilo na kumiliki ardhi hiyo baada ya Wapalestina kuondolewa.

Pendekezo hilo lilikabiliwa na hasira kutoka nchi za Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na serikali ambazo ni washirika wa Washington.

Baadaye Trump alisimamia makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalisisitiza wazi haki ya Wapalestina kubaki katika ardhi yao.

Tangu mpango wa kusitisha mapigano ulipoanza kutekelezwa mwezi Oktoba 2025, Israel imeendelea kuzuia misaada kuingia Gaza na imezuia shughuli za ujenzi mpya katika eneo hilo huku ikiendelea kufanya mashambulizi dhidi ya Wapalestina karibu kila siku.

Share This Article