Timu ya taifa ya soka Harambee Stars imenyofolewa baada ya kulazwa bao moja kwa nunge na Sudan Kusini almaarufu Bright Stars, katika pambano la kirafiki lililosakatwa Jumanne alasiri katika uga wa kimataifa wa Kasarani.
Wageni Sudan Kusini waliodhihirisha mchezo mzuri na wa kuonana walichukua uongozi kunako dakika ya tatu ya mechi kupitia kwa mshambulizi anayepiga soka ya kulipwa na klabu ya Police FC,Tito Okello akitumia vyema kosa lililofanywa na beki Joseph Okumu na kudumisha hadi kipenga cha mwisho.
Mashabiki waliitikia wito wa Rais William Ruto kujitokeza kwa wingi kuwapa shime watoto nyumbani lakini maelfu yao wakatamaushwa baada ya kipenga cha mwisho.
Kenya ilitumia pambano hilo kujipiga msasa kabla ya kuanza mechi mbili za kufuzu kwa kombe la dunia mwaka 2026 zitakazopigwa Novemba mwaka huu.
Ushinde wa Jumanne unaibua ati ati nyingi katika timu ya Kenya na kujiandaa kwake kufuzu kwa kombe la dunia baada ya kusajili ushindi wa magoli 2-1 ugenini dhidi ya Qatar Ijumaa iliyo Alhamisi ikiyopita jiji Doha.