Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula amewaonya wanasiasa dhidi ya kuingilia utendaji kazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.
Amesema jitihada za kutaka kuielekeza tume hiyo namna ya kutafuta teknolojia na vifaa vingine vya uchaguzi zitaondoa imani ya wengi kwenye tume hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Aliyasema hayo leo Ijumaa kwenye soko la Marenyo katika eneo bunge la Butere, kaunti ya Kakamega, akionekana kumjibu Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua ambaye pia ni kiongozi wa chama cha DCP.

Akiwahutubia wanahabari kabla ya kuelekea Marekani, Gachagua, miongoni mwa mambo mengine, alidai IEBC imetengeneza zabuni ya kuipendelea kampuni ya teknolojia ya Miru Systems ya Korea Kusini kwa lengo la kuwezesha udanganyifu katika uchaguzi mkuu ujao.
IEBC imekana madai hayo ikitaja mchakato wa utoaji zabuni kuwa wenye uwazi, na kwamba hakuna kampuni ambayo imepewa kandarasi hiyo kinyume cha madai ya Gachagua.
Kwa upande wake, Wetang’ula anaitaka tume hiyo inayoongozwa na Erastus Ethekon kusalia imara na kufanya kazi kwa uhuru huku akiwataka wanasiasa kukoma kuingilia kati utendaji kazi wake.
“IEBC ni taasisi huru chini ya Katiba, ikifanya kazi pasi ya maelekezo ya mtu yeyote. Wanafanya kazi yao kama inavyohitajika Kikatiba,” alisema Wetang’ula.
Alitoa mfano wa mgogoro wa uchaguzi wa urais wa mwaka 2017 ambapo Mahakama ya Juu ilifutilia mbali uchaguzi wa urais na kuagizwa kuandaa upya uchaguzi huo, akiongeza kuwa taasisi husika ziliheshimu mchakato wa kisheria.
“Sharti tuwe na heshima. Ikiwa tunaitaka IEBC ifanye kazi ipasavyo, lazima tumheshimu refa.”