Reuben Kigame amtembelea Mudavadi

Wawili hao walisema wamesalia marafiki hata ingawa wana maoni tofauti kisiasa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Kenya Reuben Kigame ametangaza kwamba jana alimtembelea mkuu wa mawaziri ambaye pia ni Waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi afisini kwake.

Kigame ambaye amewahi kuwania Urais nchini alielezea kwamba alimzuru Mudavadi kujadili masuala ya kuunda nafasi za ajira na mafunzo ya kitaaluma kwa vijana wa kaunti ya Vihiga.

“Nilikuwa na wakati mzuri na rafiki yangu Mheshimiwa Musalia Mudavadi afisini kwake nilikomtembelea kujadili uundaji wa fursa za ajira na mafunzo ya kitaaluma kwa vijana wa kaunti ya Vihiga,” aliandika Kigame kwenye akaunti yake rasmi ya Facebook.

Jingine walilojadili wawili hao ni mawazo kuhusu jinsi ya kukuza usaidizi kwa tasnia ya ubunifu nchini Kenya.

“Hata ingawa tuna maoni tofauti, tumesalia marafiki na kuendelea kubadilishana mawazo kuhusu uwezekano wa Kenya mpya,” Kigame alimalizia.

Waziri Mudavadi naye alichapisha picha za mkutano wao na kuandika, “Baadhi ya mazungumzo yenye thamani zaidi ni yale ambapo tunaweza kuwa na mitazamo tofauti, lakini bado tuchague kusikilizana, kushirikiana na kutafuta mambo tunayokubaliana”.

Aliendelea kuelezea kuridhika kwake kwa kukutana na rafiki yake, mwanamuziki maarufu wa nyimbo za Injili Reuben Kigame, “kwa mazungumzo yenye tafakuri kuhusu imani, uongozi na umoja wa kitaifa”.

Mudavadi alisisitiza kwamba Kenya inakuwa na nguvu zaidi, “tunapoendelea kuzungumza, kuheshimu tofauti zetu na kushirikiana kwa ajili ya taifa lenye amani, umoja na ustawi”.

Share This Article