KECOBO yaendelea kubana leseni ya KAMP

Mwenyekiti wa bodi ya KECOBO Joshua Kutuny alielezea kwamba KAMP haijashughulikia masuala yote yaliyoibuliwa.

Marion Bosire
2 Min Read
Joshua Kutuny, Mwenyekiti KECOBO

Bodi inayosimamia hakimiliki nchini Kenya Copyright Board, KECOBO imetangaza kwamba leseni ya Chama cha Watayarishaji wa Muziki cha Kenya, itaendelea kusimamishwa.

Katika taarifa, mwenyekiti wa bodi ya KECOBO Joshua Kutuny alielezea kwamba bodi hiyo imeamua kuchukua hatua hiyo kufuatia mkutano ulioandaliwa Agosti 24, 2026 kujadili majibu yaliyowasilishwa na KAMP.

Kutuny anasema kwamba KAMP katika majibu yake ya maswali yaliyokuwa yameibuliwa, haikushughulikia masuala yote kama inavyohitajika.

“Kwa sababu hiyo, bodi imeamua kuendelea kusimamisha leseni ya KAMP hadi wakati ambapo masuala yote yatashughulikiwa,” alielezea Kutuny.

KECOBO ilisimamisha leseni ya KAMP kuanzia Julai 1, 2026 kwa siku 90 kutokana na madai ya usimamizi duni wa fedha na utawala mbaya, na kuipa muda wa kurekebisha hali. mwenyekiti wa bodi ya KECOBO Joshua Kutuny alielezea kwamba

Iligunduliwa kwamba KAMP ilitumia shilingi milioni 5.51 za mirahaba iliyopaswa kugawiwa wasanii kwa shughuli zisizo za msingi, badala ya kuwapa wasanii fedha zao.

Chama hicho cha watayarishaji muziki kinalaumiwa kwa kuvunja sheria za bajeti kama ile ya viwango vya 70:30 vya gharama za kiutawala na kutoa ankara na leseni kwa viwango vya chini ya viwango rasmi vilivyoidhinishwa.

KAMP vile vile ilipatikana na kosa la kugawa mirahaba mwezi Juni 2026 bila kufahamisha mdhibiti na kushindwa kufuata maagizo ya awali ya bodi na makubaliano yaliyolenga kurekebisha mfumo wa utoaji leseni za muziki.

KECOBO sasa inasema kwamba inataka viongozi ambao wamekaa afisini muda mrefu waondoke mara moja na uchaguzi wa viongozi wapya uandaliwe katika muda wa siku 30.

Suala la matumizi mabaya ya zaidi ya shilingi milioni 5 sasa limewasilishwa kwa idara ya upelelezi wa jinai, DCI kwa uchunguzi.

Share This Article