Watu maarufu Uganda wakosolewa kwa mitindo duni ya maisha

Mkosoaji Frank M. Gashumba amewataka waishi maisha yanayoendana na viwango vyao vya umaarufu na hadhi katika jamii.

Marion Bosire
1 Min Read

Watu maarufu nchini Uganda wamekosolewa kufuatia kile kilichotajwa kuwa mitindo duni ya maisha.

Frank M. Gashumba ambaye ni mkosoaji mkubwa nchini Uganda sasa anatoa changamoto kwa watu hao maarufu waishi maisha yanayoendana na viwango vyao vya umaarufu na hadhi katika jamii.

Alikuwa akizungumza kwenye mojawapo ya vipindi vya majadiliano ambapo alitaja wanaojirejelea kama watu maarufu kisha wanavaa nguo kuu kuu.

Kulingana naye, watu hao wanapaswa kukoma kujirejelea kama watu maarufu iwapo hawana uwezo wa kuendana na viwango vya umaarufu.

Gashumba alitaja pia wanaopikia jiko la makaa nyumbani akisema kamwe hawastahili kujiita watu maarufu.

“Acheni kujitambulisha kama watu maarufu wakati bado mnavaa nguo za mitumba. Na kama mnajiona kuwa nyota mkipikia jiko la mkaa nyumbani, msijione kuwa mastaa hata kidogo. Mnapojipa cheo hicho, lazima muonekane na muishi kulingana nacho,” alisema Gashumba.

Jingine alilozungumzia Gashumba ni watu wanaozungumzia ndoa yake bila ufahamu kamili akisema ana mke mmoja kwa jina Patience Malaika.

Huku akikiri kwamba aliwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine awali kabla ya kuingia kwenye ndoa, Gashumba alisema marehemu babake alimshauri dhidi ya kuoa wake wengi.

Share This Article