Mashindano ya Kombe la Voliboli Afrika kwa vipusa kuanza leo Nairobi

Dismas Otuke
2 Min Read

Makala ya 22 ya mashindano ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake katika mpira wa wavu, yataanza leo Jumanne huku wenyeji Kenya – Malkia Strikers, wakiwanda taji la 11.

Jumla ya mataifa 15 yanashiriki kipute hicho kinachoandaliwa katika viwanja vya Kasarani na Ulinzi Sports Complex ambapo fainali yake itapigwa Septemba 5.

Kulingana na droo iliyoandaliwa Jumatatu jioni, Kenya imo kundi A pamoja na Mali na Zambia, wakati kundi B likisheheni Misri, Burkina Fasso,Uganda na Senegal.

Mabingwa watetezi Cameroon wamo kundi C pamoja na Nigeria,Tunisia na Ghana huku Rwanda, Algeria, DR Congo na Burundi zikiwa kundi la mwisho la D.

Makundi ya timu zinazoshiriki

Katika mechi za ufunguzi Jumanne Agosti 25, DRC watafungua kipute dhidi ya Burundi uwanjani Ulinzi kuanzia saa nne asubuhi wakati Senegal wakipambana na Uganda katika ukumbi wa Kasarani pia saa nne.

Misri watakabana koo na Burundi uwanjani Kasarani nao Rwanda wamenyane na Algeria ugani Ulinzi, mechi zote ziking’oa nanga saa sita unusu.

Mbaingwa watetezi Cameroon watachuana na Ghana saa tisa alasiri huko Kasarani wakati Niger wakiwa na miadi na Tunisia.

Wenyeji Kenya watafunga ratiba ya siku ya kwanza kwa kupimana ubabe na Zambia katika uwanja wa Kasarani kuanzia saa moja usiku, mechi ambayo itatanguliwa na sherehe za ufunguzi kuanzia saa kumi na mbili jioni.

Mabingwa wa makala ya mwaka huu watafuzu kwa mashindano ya Dunia mwaka ujao.

Share This Article