Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kile anachokitaja kuwa operesheni kali zaidi ya kiuchumi dhidi ya Iran.
Haya yanajiri wakati mazungumzo yanayolenga kumaliza vita vya zaidi ya miezi mitano kati ya nchi hizo mbili yamekwama.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye Truth Social Jumatano, Trump alisema Iran imeshindwa kutumia fursa ya kuafikia makubaliano, na kwamba itakabiliwa na vita vya kiuchumi na kutengwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Pia alitishia kuweka vikwazo dhidi ya nchi yoyote inayofanya biashara na Iran.
“Nchi yoyote inayoruhusu taasisi zake za kifedha, biashara, viwanja vya ndege au taasisi za serikali kutoa aina yoyote ya msaada kwa Iran, yenyewe itakabiliwa na MADHARA MAKUBWA ya kiuchumi,” aliandika Trump.
Alitaja pia usafirishaji haramu wa mafuta, mikataba ya kubadilishana fedha, uhamishaji wa fedha taslimu, maduka ya kubadilisha fedha, usajili wa meli, kampuni zinazotumika kuficha shughuli akisema yote hayo yanapaswa kukoma sasa.
“Mnajijua. Hii itakuwa siku ya kiama ya kiuchumi, na tunahitaji washirika wetu wote kusimama pamoja na Marekani ili kuitenga na kuishinda tishio la Iran,” aliandika.
Hii si mara ya kwanza kwa Trump kuitishia Iran vikwazo vya kiuchumi.
Utawala wake umeendesha kampeni ya shinikizo dhidi ya Iran tangu Aprili chini ya kaulimbiu ya Operation Economic Fury, iliyolenga kuitenga Tehran na kuzuia vyanzo vyake vya mapato.
Hakukuwa na jibu la haraka kutoka kwa maafisa wa Iran, lakini vyombo vya habari vya Iran vilipuuza tangazo la Trump, vikisema kuwa halikuwa na jambo jipya.