Bunge la kitaifa limepitisha mswada wa michezo wa mwaka 2026 uliofanyiwa marekebisho ambao unapendekeza adhabu kali dhidi ya makosa ya upangaji matokeo ya mechi katika michezo humu nchini.
Mswada huo uliowasilishwa na Mbunge mteule Irene Nyakerario Mayaka,unalenga kuimarisha uadilifu michezoni humu nchini kwa kuharamisha vitendo vyote vinavyohujumu uadilifu michezoni.
Baadhi ya vipengee muhimu katika mswada huo ni ubainishaji wa kisheria kuhusu upangaji matokeo katika michezo huku kosa hilo likijumuisha kupokea au kutoa fursa ya mapendeleo ambayo itabadilisha matokeo ya mchezo na kutumia taarifa za ndani ya timu au kikosi kwa minaajili ya kutumika kwa uchezaji kamari.
Aidha,sheria hiyo itaimarisha jukumu Halmashauri ya michezo nchini ambapo sasa watakuwa na uwezo wa kupokea taarifa na ripoti kuhusu visa vinavyoshukiwa vya upangaji matokeo na kufanya uchunguzi kwa ushirikiano na taaisi husika.
Uchunguzi wote kuhusiana na upangaji matokeo ni sharti ukamilike ndani ya kipindi cha miezi sita .
Pia mswada huo umetanua majukumu ya jopo la kutatau migogoro ya michezo nchini ambapo litaskiza rufaa zinazohusiana na madai ya upangaji matokeo katika michezo.
Watakaopatikana na hatia ya kuhusika katika upangaji matokeo watatozwa faini ya shilingi milioni 1 au kuhukumiwa kifungo kisichozidi mwaka mmoja au adhabu zote mbili.
Aidha, timu zitakazopatikana na hatia ya kupanga matokeo ya mechi zitapokonywa alama zote za mechi hiyo na pia watu binafsi watapoteza mchezo pamoja na kufurushwa mashindanoni au hata kupigwa marufuku ya maisha .
Pia timu au watu watakaopatikana na hati ya kupanga matokeo michezoni watapokonywa pesa walizopata kupitia uhalifu huo.