Lissu kufahamu hatima yake Ijumaa

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dar es salaam itaamua siku hiyo, iwapo ana kesi ya kujibu au la.

Marion Bosire
2 Min Read
Tundu Lissu, Kiongozi CHADEMA

Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu anatarajiwa kufahamu hatima yake, kuhusiana na kesi inayomkabili ya uhaini, Ijumaa Agosti 21, 2026.

Kesi hiyo ya uhaini imeahirishwa hadi Ijumaa Agosti 21, 2026 siku ambayo Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dar es salaam itatoa uamuzi kuhusu iwapo ana kesi ya kujibu au la.

Jopo la Majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru limesema linahitaji muda kuandaa uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za Lissu na Upande wa Jamhuri pamoja na kupitia ushahidi wa Mashahidi 17 uliowasilishwa na Upande wa Mashtaka.

Awali katika hoja zake, Lissu aliambia Mahakama kuwa hana kesi ya kujibu, huku akiitaka itamke kuwa hana hatia na kuamuru alipwe fidia.

Akirejea maamuzi mbalimbali ya Mahakama, ikiwemo kesi ya Rambaklal Trambaklal Bhatt dhidi ya Jamhuri, Lissu amesema katika shtaka la uhaini lazima kuwe na uthibitisho wa nia ya kufanya kitendo hicho na nia hiyo inapaswa kuthibitishwa kupitia maandishi au matendo ya wazi.

Lissu amekuwa kizuizini tangu Aprili 9, 2026, punde baada ya mkutano wa kisiasa wa CHADEMA mjini Mbinga, kusini mwa Tanzania, kabla ya kufunguliwa mashtaka ya uhaini kesho yake.

Haya yanaaminika kutokana na kampeni ya chama chake ya kuhimiza mabadiliko almaarufu, “No reform, No election”.

Share This Article