Uchaguzi wa Zambia: Hakainde Hichilema achukua uongozi wa mapema

Kulingana na katiba ya Zambia, ili kutangazwa Rais, ni sharti mgombea apate asilimia 50 ya kura zote ili kuepuka raundi ya pili ya upigaji kura.

Dismas Otuke
1 Min Read

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amechukua uongozi wa mepema kwenye matokeo ya uchaguzi mkuu wa wiki jana na kumweka katika nafasi bora ya kushinda Urais kwa muhula mwingine katika raundi ya kwanza ya upigaji kura.

Shughuli ya kuhesabu kura ilianza Alhamisi wiki iliyopita punde baada ya kufungwa kwa vituo vya kupiga kura na zaidi ya nusu ya kura za maeneo bunge zilikuwa zimehesabiwa kufikia jana Jumapili.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi nchini Zambia, matokeo ya awali yaliashiria uongozi mkubwa wa Hichilema wa chama cha United Party for National Development (UPND) wa asilimia 59 ya kura zote zilizohesabiwa.

Mpinzani wake wa karibu Brian Mundubile wa chama cha National Reconciliation Party for Unity and Prosperity (NRPUP), alifuata kwa mbali akiwa na thuluthi moja tu ya kura zilizohesabiwa.

Kulingana na katiba ya Zambia, ili kutangazwa Rais, ni sharti mgombea apate asilimia 50 ya kura zote ili kuepuka raundi ya pili ya upigaji kura.

Kura hizo zimekumbwa na utata huku jumuiya ya kimataifa ikimshutumu Hichilema kwa kile ilichokitaja kuwa kampeni zilizoegemea upande mmoja zilizolenga kuukandamiza upinzani.

Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa wakati wowote wiki hii.

Share This Article