Huenda huduma muhimu za kaunti ya Nairobi zikalemazwa endapo wafanyakazi watatekeleza vitisho vyao vya kugoma wiki hii kulalamikia kucheleweshwa kwa mshahara wa mwezi Julai.
Wafanyakazi hao waliapa kuanza mgomo juma hili endapo mishahara yao haingelipwa kufikia leo Jumatatu, Agosti 17.
Gavana Johnson Sakaja alitoa hakikisho wiki jana kuwa mchakato wa kutuma mishahara kwa akaunti za benki za wafanyakazi ulikuwa umeanza na kuwataka kuwa na subira.
Endapo mgomo huo utaanza, huenda huduma kama vile uzoaji taka, huduma za zima moto, usafishaji barabaraba za mijini na huduma nyinginenezo zikasitishwa na kusababisha kero kubwa.
Wafanyakazi takriban 19,000 wa kaunti ya Nairobi hawakuwa wamelipwa mishahara yao ya mwezi Julai kufikia Ijumaa iliyopita.