Mwigizaji mkongwe wa tamthilia, mwandishi na mtengenezaji filamu kutoka Uganda, Alex Mukulu, amefariki akiwa na umri wa miaka 72.
Kifo chake kinahitimisha safari ya kazi iliyosaidia kuunda sura ya uigizaji wa kisasa nchini humo na kiliripotiwa jana Jumamosi na vyombo vya habari vya Uganda.
Chanzo cha kifo chake hata hivyo hakikuwekwa wazi.
Mukulu alizaliwa mwaka 1954 huko Misebe, Kaunti ya Ssingo, Buganda na kusomea filamu na uigizaji katika Chuo Kikuu cha Makerere baada ya kusoma katika Shule ya Sekondari ya Kololo.
Alifahamika sana kwa kutumia maigizo kuwasilisha malalamishi, akitumia kazi zake kuchunguza mabadiliko ya kisiasa, ukosefu wa usawa kijamii, utamaduni na maisha ya kila siku nchini Uganda.
Miongoni mwa kazi zake mashuhuri ni Wounds of Africa ya mwaka 1988, 30 Years of Bananas ya mwaka 1991, Excuse Me Mzungu ya mwaka 1992 na The Guest of Honour ya mwaka 1994.
Tamthilia yake ya Journey to Self-Realization iliwasilishwa katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Kampala mwaka 2007.
Alirejea jukwaani mwaka 2024 baada ya mapumziko marefu na tamthilia iitwayo Kulunkalu ne Kulumbisi, ambayo ni uigizaji wa Kiafrika wa tamthilia ya Romeo and Juliet ya William Shakespeare.
Kupitia kazi zake, Mukulu mara nyingi alitumia jukwaa kuwapa watazamaji changamoto kuhusu masuala ya kisiasa na kijamii.
Mukulu ameacha urithi mkubwa katika tamthilia, uliounganisha burudani na maoni kuhusu jamii, huku ukiwasukuma watazamaji kutafakari hali halisi ya kisiasa na kitamaduni nchini humo.
Maelezo kuhusu mipango ya mazishi yake pamoja na taarifa zaidi kutoka kwa familia yake yanatarajiwa kutangazwa baadaye.