Mulo asema angetaka mirabaha ya densi zake

Mbali na fedha, Mulo anafurahia kuona miondoko yake ikichezwa kwenye majukwaa ya kimataifa.

Marion Bosire
1 Min Read

Mtaalamu wa mitindo ya densi nchini Uganda, Mulo Mazzina, amezungumzia hisia za kutaka kutuzwa kwa ubunifu wake baada ya kuona watu maarufu wakicheza baadhi ya miondoko yake maarufu ya densi.

Mazzina alikuwa akijibu swali kuhusu iwapo kuna mtu aliyewahi kunakili au kucheza miondoko yake ya densi na kumfanya ahisi kwamba anapaswa kumlipa pesa.

Alitaja wachezaji wa Uganda Cranes na wa timu ya taifa ya netiboli nchini humo, ambao amewaona wakionyesha miondoko yake ya densi wakati wa mashindano ya kimataifa.

Alisema angekuwa na mawasiliano na wasimamizi wa wanamichezo hao, angehitaji walipie matumizi ya kazi yake ya ubunifu.

Hata hivyo, alikiri kwamba mbali na suala la kifedha, kuona miondoko yake ikichezwa kwenye majukwaa ya kimataifa pia humletea furaha kubwa, hasa katika maeneo ambayo bado hajafika.

Hata hivyo, Mazzina alisisitiza kwamba bado angefuatilia madai yake ikiwa angeweza kuwasiliana na watu wanaowajibika kwa wanamichezo hao.

Mtaalamu huyo wa densi pia alikumbuka kumuona Waziri Mkuu na Kiongozi wa Shughuli za Serikali, Robinah Nabbanja, akicheza baadhi ya miondoko yake ya densi.

Kwa utani, alisema kwamba hata watu mashuhuri wa kiwango hicho wanapaswa kufikiria kumtuza kwa ubunifu uliotumika kuunda miondoko hiyo.

Share This Article