Wakenya wahimizwa kutoingiza siasa kwenye miradi ya maendeleo

Kindiki aliwahimiza Wakenya kujiamini na kuhakikisha sera za taifa hili hazivurugwi.

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakenya wahimizwa kutoingiza siasa kwenye miradi ya maendeleo.

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, ametoa wito kwa Wakenya kutoingiza siasa kwenye miradi ya maendeleo, akidokeza kuwa hatua hiyo huenda ikahujumu malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mdahalo wa kitaifa kuhusu ruwaza ya mwaka 2060 katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC), Nairobi, Kindiki aliwahimiza Wakenya kujiamini na kuhakikisha sera za taifa hili hazivurugwi.

Huku akisema uchumi wa taifa hili umeimarika, Naibu huyo wa Rais aliwata Wakenya kutokuwa na dhana kwamba maendeleo yanaweza tu tekelezwa katika mataifa mengine, akihimiza kuwa mataifa ya Afrika yana uwezo wa kukabiliana na umaskini na kutimiza maendeleo endelevu.

“Tunapaswa kujiamini ya kwamba tuna uwezo wa kutekeleza yale mataifa mengine yanatekeleza ili kuondoka katika hali ya umaskini hadi hali ya ufanisi,” alisema Prof. Kindiki.

Kulingana na Kindiki, mdahalo kuhusu ruwaza ya mwaka 2060, unatoa fursa kwa Kenya kukadiria hatua ilizopiga za maendeleo na kutafakari kile inachopaswa kutekeleza ili kuafikia viwango vya juu vya maendeleo.

Share This Article