Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, amesema kuwa ili taifa hili liweze kufikia viwango vya mataifa yaliyostawi, ni shati lipunguze mikopo ya nje ya nchi, livutie uwekezaji wa kimataifa na litumie ushirikiano wa serikali na sekta ya kibinafsi kuboresha miundombinu.
Kulingana na Mudavadi, ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege na viwanja, haubainishi maendeleo, ila udhabiti, mshikamano wa kitaifa na rasilimali za kiuchumi, akidokeza zinawapa wawekezaji ujasiri, zinalinda maisha na kufanikisha biashara kustawi, huku familia zikipata fursa ya kupanga mustakabali wao.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, aliyasema hayo kwenye kongamano la kitaifa kuhusu ruwaza ya mwaka 2063, lililoandaliwa katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC), Jijini Nairobi.
“Tunapoangazia mwaka 2063, wakati Kenya itatimiza miaka 100 tangu kujipatia uhuru, ruwaza hii haiwezi milikiwa na serikali pekee,” alisema Mudavadi.
Mjadala huo wa kitaifa ulioongozwa na Rais William Ruto, uliwaleta pamoja Wakenya wa tabaka mbali mbali kubuni malengo ya maendeleo baada ya ruwaza ya mwaka 2030.
Wakenya wamehimizwa kutoa mawazo na suluhisho ambazo zitaboresha taifa hili na kufaidi vizazi vijavyo.