Ruwaza 2060 itakayoongoza maendeleo ya taifa kuzinduliwa Jumatano

Uzinduzi wa "Mazungumzo ya Kitaifa: Baada ya 2030," unatarajiwa kufanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC kuanzia majira ya saa mbili asubuhi. 

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akihutubia taifa Julai 30, 2026

Mjadala kuhusu mustakabali wa maendeleo ya kitaifa nchini unatarajiwa kuanza rasmi kesho Jumatano wakati Rais William Ruto atakapoliongoza taifa kuzindua Ruwaza 2060. 

Uzinduzi wa “Mazungumzo ya Kitaifa: Baada ya 2030,” unatarajiwa kufanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC kuanzia majira ya saa mbili asubuhi.

Akihutubia taifa Julai 30 mwaka huu, Rais Ruto alipendekeza Ruwaza 2060 aliyoitaja kuwa mkataba wa kitaifa wa maendeleo aliyoutaja kuwa mwongozo wa kikatiba.

Ruto akitumia fursa hiyo kuwaambia Wakenya kuwa lengo lake kuu ni kuipa mipango ya maendeleo ya taifa msingi wa kisheria ndani ya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010.

Mabadiliko hayo ya kimuundo yanalenga kulinda malengo ya maendeleo ya uchumi wa taifa dhidi ya mabadiliko ya vipaumbele, ilani za kisiasa na maslahi yanayobadilika.

Baadhi ya viongozi wa upinzani wamepuuzilia mbali mkataba wa maendeleo uliopendekezwa na badala yake kuutaka utawala wa Kenya Kwanza kutimiza ahadi za kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 kabla ya kuzungumzia maendeleo ya muda mrefu.

Hata hivyo, upande wa serikali umeushutumu upinzani kwa ukosoaji wake ukisisitiza umuhimu wa nchi kuwa na mwongozo wa muda mrefu wa kuleta mageuzi ya kiuchumi na kujenga mustakabali wenye heshima zaidi kwa Wakenya.

Akizungumza siku moja kabla ya uzinduzi wa ruwaza hiyo, Waziri wa Fedha John Mbadi alisema wakati umewadia wa kuzungumzia Kenya itakavyoendelezwa baada ya kukamilika kwa Ruwaza 2030.

“Nimesiki watu wakisema, “Mbona Ruto ameunda ruwaza nyingine?” Ruto hajaunda ruwaza nyingine. Kesho, tunaanza mjadala mwingine kuhusu namna ya kuunda ruwaza ya nchi hii. Hilo linapaswa kubainika vilivyo,” alisema Mbadi.

“Ruwaza 2060 si ya William Ruto. Ruto anaweza tu kuwa madarakani hadi mwaka 2032, siyo zaidi ya hapo. Hivyo, hii si ruwaza yake. Atatekeleza sehemu ndogo mno ya ruwaza hiyo.”

Wakenya wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ushirikishwaji wa umma mara tu ruwaza hiyo itakapozinduliwa, kwani maoni yao yatasaidia kuunda mfumo wa maendeleo utakaorithi Ruwaza 2030.

Azima ya serikali ikiwa ni kufikia  mwongozo wa kitaifa wa maendeleo unaoakisi matarajio ya Wakenya wote.

 

Share This Article