Serikali ya Uganda imeelekeza baa na maeneo ya kuuza pombe ya kienyeji kufunguliwa baada ya saa 9 alasiri siku za kazi, huku ikiimarisha udhibiti wa unywaji pombe kwa walio chini ya umri wa miaka 18, kamari na uwajibikaji wa serikali za mitaa.
Hii ni sehemu ya hatua zinazotekelezwa na serikali hiyo kwa lengo la kupunguza unywaji pombe asubuhi na kuongeza tija.
Waziri wa Serikali za Mitaa nchini humo, Balaam Barugahara Ateenyi, alitoa agizo hilo kwa wenyeviti wa LC5, mameya wa miji, mameya na wenyeviti wa mabaraza leo Agosti 11, 2026.
Kwa mujibu wa agizo hilo, baa, maeneo ya pombe ya kienyeji na sehemu nyingine zinazouza vileo hazipaswi kufunguliwa kabla ya saa 9 alasiri siku za kazi, kwa kuzingatia sheria za kitaifa, masharti ya leseni na kanuni halali za serikali za mitaa.
Barugahara alisema viongozi wa mitaa wanapaswa kushirikiana na vyombo vya usalama na makundi ya utekelezaji wa sheria ili kukomesha unywaji pombe wa asubuhi.
Alisema unywaji wa pombe kupita kiasi huchangia uvivu, matatizo ya kifamilia na uhalifu katika jamii.
Waziri huyo pia alizielekeza mamlaka kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wamiliki wa baa, wauzaji wa madukani na waendeshaji wa maeneo ya malwa wanaowauzia au kuwapatia pombe watu walio chini ya umri wa miaka 18.
Agizo hilo pia linazitaka serikali za mitaa kudhibiti saa za uendeshaji wa kampuni za kamari ndani ya maeneo yao ya mamlaka.
Barugahara alisema hatua hiyo inalenga kulinda jamii, hasa vijana, dhidi ya madhara yanayohusishwa na kamari kupita kiasi.